Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mheshimiwa Angellah Kairuki, leo, Agosti 3, 2020 ametembelea banda la PPRA katika Maonesho ya 27 ya Wakulima maarufu kama Nanenane yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu.
Waziri Kairuki ameitaka PPRA kuendelea kuzisimamia taasisi nunuzi ili kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya zabuni zinazotolewa kwa makundi maalum, ambazo ni 30% ya ununuzi wake, kama sheria ya ununuzi wa umma inavyoelekeza.
Makundi maalum ni pamoja na wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
“Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 na sheria pia inazitaka taasisi nunuzi kutenga 30% kwa ajili ya makundi maalum, PPRA mnapaswa kuhakikisha mna -mechanism ya kufuatilia utekelezaji wake. Tuliwaahidi wananchi, tusimamie utekelezaji wake,” amesema Waziri Kairuki.
Kanuni ya 30A hadi 30D, ya Kanuni za Sheria ya Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 na marekebisho yake ya mwaka 2016, inazitaka taasisi nunuzi kuyapa fursa makundi maalum kwa kutenga 30% ya ununuzi wa taasisi kwa ajili ya makundi maalum.