Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, ametoa siku tisa kwa Bandari ya Dare es Salaam kuhakikisha Transforma sita zilizopo katika bandari hiyo kusafirishwa kwenda kwenye ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere JNHPP.
Ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye Badari hiyo na kuwapa mpaka Tarehe 12 wawe wameshazifikisha Transforma hizo kwenye mradi.
Aidha Katika ziara hiyo, aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.
Dkt. Kalemani,amesema lengo la ziara ni kujua sababu ambazo zimepelekea kucheleweshwa kwa kuondolewa kwa Transfoma hizo katika bandari hiyo, ambapo zinatakiwa kupelekwa katika mradi wa Julius Nyerere ili kuendelea na ujenzi wa mradi huo.
Amesema mwezi uliopita alipotembelea mradi wa Julius Nyerere alihakikishiwa kuwa transfoma hizo zitafika kwa wakati katika mradi huo lakini bado hazijapelekwa.
“ Hizi Transfoma zimekwamishwa na nini , kwanini zimalize mwezi mzima bandarini na wakati zilitakiwa ziwe zimetoka naomba niseme sitavumilia hii hali, huu mradi wenyewe ni wa haraka haraka kila mmoja anauhitaji kwahiyo hatutavumilia mtu yoyote atucheleweshe,”Amesema Waziri Kalemani.
Aidha, amewataka waatalamu wote ambao wanaohusika na nyaraka ambazo zinahusika na uletaji wa vifaa nchini, wakizipata nyaraka hizo waanze mara moja na taratibu zote za utoaji wa mizigo bandarini.
Pia, amewataka watumishi wa bandari kutoa ushirikiano kwa Wizara ili kuweza kutatua changamoto zozote ambazo zitajitokeza na kuwataka kuwasiliana na viongozi wa Wizara ili kumaliza changamoto hizo kwa haraka.