Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuweka alama zinazoonekana kuzunguka eneo la mradi wa Kuchakata na kusindika Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Likong’o wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi.
Waziri Kalemani ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na wawekezaji wa mradi huo, kampuni ya Equinor na Shell.
“ Eneo tumeligharamia hivyo ni muhimu likawekwa alama zinazoonekana badala ya kuweka bango pekee ili eneo hili liweze kutambulika na wananchi wasije kulivamia au kutumika vibaya, hivyo tuna wajibu wa kulinda eneo hili na kuonesha kuwa kuna kazi inakuja.” Amesema Dkt.Kalemani
Aidha, Dkt. Kalemani ametoa agizo kwa TPDC, ndani ya siku Tano wawe wamekamilisha taratibu za upatikanaji wa mkandarasi kutoka mkoani Lindi atakayeweka alama hizo za mipaka na mkandarasi huyo aanze kazi mara moja.
Waziri Kalemani amewaeleza wadau hao kuwa, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 5.72 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa eneo hilo kazi ambayo ilikamilika mwaka jana.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, alisema kuwa Serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi mkoani Lindi kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kujiletea maendeleo.