Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka wananchi kutunza miundombinu ya Umeme inayopita katika vijiji vyao.

Akizungumza katika Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Kalemani amesema kuwa serikali inatumia gharama kubwa kufikisha umeme na kuwataka wananchi wasifanye shughuli zitakazo athiri miundombinu ya Umeme ikiwemo kuwasha moto karibu na nguzo na badala yake wahamasike kulipia huduma ya Umeme ili iweze kuwasaidia katika shughuli zao za kiuchumi

Akiwasha umeme katika vijiji vya Nanditi na Mombaka katika Wilaya ya Masasi, Kalemani amezitaka halmashauri za wilaya, kulipia gharama za Umeme za taasisi mbalimbali za kijamii ikiwemo Shule na zahanati na kudai umeme mara tu baada ya kulipia

“Kabla ya kulalamika shule haina umeme na zahanati haina umeme, jiulize swali moja tu umelipia? lipia kwanza ndo udai umeme, halmashauri zote za wilaya lipieni taasisi za umma, tunataka wananchi wapate umeme, na umeme pia ufike mashuleni, zahanati, na sehemu zote zinazotoa huduma,”amesema Kalemani

Aidha, Dkt. Kalemani amemtaka Mkandarasi kukamilisha kuunganisha umeme katika vijiji 122 vilivyobaki katika kata ya Mndibwa, ndani ya siku 25.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Masasi, Selemani Mzee ameishukuru Serikali kwa kufikisha Umeme Masasi na kuwataka wananchi wote wa masasi kulipia Umeme.

JPM afanya uteuzi
Mabweni ya shule ya Wasichana Ashira yateketea kwa moto