Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amewafukuza kazi na kuwataka kuondoka nchini mara moja wafanyakazi wawili wa kampuni ya China New Railway 15 Bureau Group Corporation inayojenga barabara ya Chunya –Makongolosi Km 39 kwa kiwango cha lami kwa kukiuka mkataba na kudhalilisha wafanyakazi.

Wafanyakazi hao ni Meneja mradi, Pen Pong na Meneja rasilimali watu, Liun Migun ambao kwa pamoja licha ya kukiuka vipengele vya mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo pia wanatuhumiwa kuwapiga na kuwafukuza kazi wafanyakazi wakitanzania kwa uonevu.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Matundasi wilayani Chunya Mhandisi, Kamwelwe amesema kuwa haiwezekani Serikali ikamvumilia mkandarasi asiyezingatia mkataba na anayedhalilisha wananchi ambao ndio walipa kodi zinazotumika kumlipa na kuwaonya makandarasi wote nchini kuzingatia mikataba na kutenda haki kwa wafanyakazi wao.

Amesema kuwa barabara ya Chunya –Makongolosi Km 39,  ambayo ujenzi wake ulitakiwa kuanza Oktoba 30 mwaka 2017 na kukamilika Januari 2020 hadi sasa imejengwa kwa asilimia 13 badala ya 20 zilizokubaliwa katika mkataba.

Aidha amesema mkandarasi wa China New Railway 15 Bureau Group Corporation amekiuka mkataba kwani alitakiwa awe na mitambo75 kwaajili ya ujenzi na hadi sasa ni mitambo 34 tu inayofanyakazi, awe na wataalam saba na hadi sasa ni wataalam watatu tu wanaofanyakazi licha ya kulipwa asilimia 15 ya malipo ya awali.

“Natoa miezi mitatu kwa kampuni hii kujirekebisha na kuzingatia mkataba kabla hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa,” amesema Waziri Kamwelwe.

Hata hivyo, katika hatua nyingine Waziri Kamwelwe ametoa mwezi mmoja kwa mkandarasi wa China Civil Engineering Corporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga –Nyigo Km 74.1 na Nyigo –Igawa Km 63.8 kukamilisha ujenzi huo  kwa mujibu wa mkataba.

 

Aweso awatangazia kiama watakao tafuna fedha za mradi
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 6, 2018