Waziri MKassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) kulishughulikia suala hilo.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo Mei 5, 2022 wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa Wiki ya Ununuzi wa Umma iliyoanza leo katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC, jijini Arusha.

“Pamoja na uwepo wa taasisi zinazosimamia manunuzi yanayofanywa katika ofisi zetu, bado wasimamizi wa manunuzi hawajaona huruma kwa walipakodi wetu kwa kuendelea kufanya manunuzi kwa gharama kubwa,” amesema Waziri Mkuu na kutolea mfano manunuzi yaliyofanywa na maafisa manunuzi wa MSD ambao wamenunua vifaa kwa gharama kubwa tofauti na bei halisi ya soko.

Amesema kupitia fedha ya UVIKO-19 ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alienda kukopa nje, ilitolewa fedha kupitia Wizara ya Afya ili zinununue vifaa vya tiba kwa ajili ya hospitali za mikoa, za rufaa, vituo vya afya na zahanati kwa nia ya kuwapunguzia mzigo Watanzania wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za tiba.

“MSD ilipata mgao wa fedha na ilipaswa kununua baadhi ya vifaa na nataka nitoe mfano huu: Walipaswa kununua kipimo cha sukari (blood glucose test) kwa sh. 150.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 300.00. Walipaswa kununua kifaa cha kupima mkojo (urinalysis) kwa sh. 200.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 780.00”

“Walitakiwa kununua kipimo kidogo cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 2,100 lakini wao walikinunua kwa sh. 4,500; pia walitakiwa kununua kipimo kikubwa cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 3,800 lakini wao walikinunua kwa sh. 6,300; na walitakiwa kununua kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo na ini (Renal and Liver Function Test) kwa sh. 6,000 lakini wao walikinunua kwa sh. 40,000.”

Waziri Mkuu amesema MSD walipaswa kununua mashine ndogo ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-semi automated) kwa sh. 1,357,200.00 lakini wao waliinunua kwa sh. 6,786,000 ilhali mashine kubwa ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-full automated) iliyopaswa kununuliwa kwa sh. 10,530,000.00 wao waliinunua kwa sh. 49,000,000.

“Walipaswa kununua mashine kubwa ya kupimia hematolojia ya mwili (hematology analyzer 5-part dff full automated) kwa sh. 20,826,000 lakini wao waliinunua kwa sh. 117,000,000. Walipaswa kununua mashine ya kupima mfumokinga wa mwili (Immunology Analyzer Full Automated) kwa sh. 37,440,000.00 lakini wao waliinua kwa sh. 149,760,000.00; na mashine ya kuchata maji kwa ajili ya kutumika katika kusafisha damu walipaswa kuinunua kwa sh. 32,660,880.00 lakini wao waliinunua kwa sh. 129,000,000.00.”
 
“Sasa wataalamu wa manunuzi mtuambie, hii inatokea kwa sababu ya nini? Na kwa maslahi ya nani?” aamehoji na kuongeza “Haya yanafanywa na watu wachache wasiokuwa na nia njema kwa fedha za walipakodi wa Tanzania. Tungeweza kupata vifaa vingi lakini tumenunua kifaa kimoja tu kwa sababu kuna mtu mmoja anatukwamisha kwa kununua bidhaa hii moja kwa bei ya juu.”
 
“Niambieni ni kweli aliyepokea fedha hizo bado anazo? Je huyu aliyeendesha hilo zoezi hajaenda kufuata fedha nyingine? PSPTB wamesema kazi yao ni kuchukua hatua kwa watumishi wanaokiuka maadili ya taaluma hii. Hatuwezi kukubali fedha za kununua vifaa halafu mtu mmoja ananunua kifaa cha shilingi milioni 12 kwa shilingi zaidi ya milioni 100! Hebu nenda kaangalie.”
 
Waziri Mkuu amesema usimamizi uliofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) umeokoa kiasi cha shilingi bilioni 98.16 lakini zipo kasoro nyingi zinazohusu ununuzi, usimamizi wa miradi na matumizi mabaya ya fedha za miradi zilizoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa yake ya mwaka 2020/2021.

Rais Samia kupokea Kombe la Dunia
TARURA yaondolewa kukusanya ushuru wa maegesho