Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuonya Mwanaharakati, Cyprian Musiba akimtaka asiwaaminishe watanzania kuwa anatumwa na viongozi wa Serikali.

Akizungumza leo jijini Dodoma, Waziri Lugola amesema kuwa Musiba anafanya harakati kama wanaharakati wengine na amewataka Watanzania kutoamini kuwa harakati zake zina uhusiano wowote na Serikali.

“Nitumie fursa hii kumuonya mwanaharakati huru Cyprian Musiba ambaye mara kadhaa amekuwa akijaribu kuonesha au kuwaaminisha Watanzania kwamba pengine Serikali inamtuma, au pengine Rais amemtuma,” amesema Waziri Lugola.

“Nataka kuwahakikishia Watanzania kwamba Serikali haiwatumi wanaharakati, wanaharakati wanafanya uanaharakati lakini wasifanye uanaharakati kwa kupitiliza kwa kujaribu kuwaaminisha Watanzania kwamba viongozi wanabariki uanaharakati wao,” aliongeza.

Aidha, Waziri Lugola alikumbushia waraka ulioandikwa na baadhi ya viongozi wa dini ambao alidai walionesha wasiwasi wao kuwa huenda analindwa kwa namna moja au nyingine vitendo vyake vina baraka za Serikali.

“Serikali haimjui Cyprian Musiba,” alisema Lugola, na kuongeza, “ endapo Jeshi la Polisi tutabaini kwamba Cyprian Musiba anaendelea kujiwasilisha katika mazingira yanayoashiria kuwajengea hofu Watanzania kwamba maneno anayosema au shughuli zake anazozifanya za kiuanaharakati tutachukua hatua kali bila kutazamana usoni na bila kuoneana huruma.”

Lugola amewata Watanzania kufahamu kuwa kama kuna mtu alikuwa akijaribu kuwaaminisha kuwa Musiba ana uhusiano wowote na viongozi Serikalini wanapawa kumpuuza.

Hizi hapa nafasi za kazi kutoka makampuni 10 Tanzania
Mbunge ataka sheria kuwabana wanaotoa ushuzi ndani ya ndege