Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaweka kwenye mzani na kuwachambua wasanii wanaochuana kwenye orodha A ya kiwanda cha muziki wa kizazi kipya, Diamond na Ali Kiba akigusa kona ya tabia zao.
Lugola ambaye amejitanabaisha kama mmoja kati ya wadau wa muziki wa kizazi kipya, amesema kuwa anawafuatilia wasanii hao ambao wanachuana vikali lakini amedai Diamond Platnumz hana nidhamu tofauti na Ali Kiba ambaye amesema anayo nidhamu ya kazi.
“Ali Kiba na Diamond… mimi niwashindanishe kinidhamu. Ali Kiba ana discipline (nidhamu); na Diamond aliwahi kulalamikiwa na wenzetu kwamba amekuwa akichelewa kwenye jukwaa,” Waziri Lugola ameiambia Mwananchi Digital.
“Unaweza kuwa na muziki mzuri wa kumuinua mtu kwenye kiti lakini mashabiki unaweza ukawaudhi kwa kutotokea jukwaani mapema japo una muziki mzuri na wakakuona wewe sio mzuri,” aliongeza.
Hata hivyo, aliomba kutojibu ni nani zaidi kati ya wasanii hao akieleza kuwa kwakuwa wanachuana tuendelee kuwapa muda angalau mwaka mmoja tutapata matokeo.
Katika hatua nyingine, Waziri Lugola aliwataja Aslay na Beka waliokuwa sehemu ya Yamoto Band kuwa ndio wasanii wanaolikuna sikio lake zaidi na kumfanya acheze kidogo anaposikia nyimbo zao.
Lugola anayefahamika kama mbunge machachari aliyewahi kuvaa vazi la Ninja ndani ya Bunge ili ‘awaue wanaoharibu bila kuwaangalia usoni’, aliteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichua nafasi ya Dkt. Mwigulu Nchemba.