Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki Nchini, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, January Makamba anatarajiwa kuzindua operesheni ya ukusanyaji wa mifuko ya Plastiki kwa hiyari kabla ya tarehe moja juni.
Waziri Makamba anatarajiwa kushiriki operesheni hiyo ambayo itaanza kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam kwa kuzungukia wauzaji wakubwa wa mifuko ya plastiki “supermarkets”, na maeneo mengine yenye matumizi makubwa ya mifuko hiyo.
Kwa upandewake Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema ukusanyaji wa hiyari wa mifuko ya plastiki katika wilaya yake utaanza mei 27 hususan katika maeneo ya Kariakoo, Buguruni, na Ukonga ambapo wataongozana na Waziri Makamba na watatumia fursa hiyo kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya mifuko ya Plastiki.
Aidha amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kuwapa onyo wale watakao jaribu kukaidi kwa makusudi au kuhujumu zoezi hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Ofisa Mawasiliano, Habari na Uhusiano wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Innocent Byarugaba ametoa taarifa kwa waandishi wa habari kuwa wafanyabiashara wote mjini kibaha wanatakiwa kutumia vifungashio na mifuko rafiki kwa mazingira ili kujiepusha na adhabu ya faini ya sh.30,000 au kifungo cha wiki moja jela.