Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemshukuru mchezaji wa Young Africans, Aziz Ki kwa zawadi ya mpira wa Hat Trick, baada ya mchgezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Benjain Mkapa, Dar es Salaam juzi Jumatatu (Oktoba 23).

Kuonesha kushukuru kupewa zawadi hiyo, Mavunde anayefahamika kwa ushabiki wake kwa mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Ahsante sana rafiki yangu Aziz Ki kwa zawadi hii ya mpira.

“Uliniambia nije uwanjani una zawadi yangu, sikukujulisha kama nakuja uwanjani ili nikusurprise nikaishia kuwa surprised mimi.”

Pia Mavunde amempongeza kiungo huyo wa kimataifa wa Burkina Faso kwa kuonesha kiwango bora kwenye mchezo huo na kuisaidia timu yake kuondoka na pointi tatu ambapo sasa inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara.

Aziz Ki aliyejiunga na Young Africans msimu wa mwaka 2021/22 akitokea miamba ya soka ya Ivory Coast, ASEC Mimosas amekuwa mwiba mchungu kila akikutana na Azam ambapo mpaka sasa ameifunga timu hiyo mabao matano.

Mchezo wa marudiano kwenye ligi msimu uliopita dhidi ya Azam, Aziz Ki aliifungia Young Africans bao la pili na kuhusika kwenye mabao mengine mawili kwenye ushindi wa mabao 3-2 waliopata dhidi ya timu hiyo.

Ki alifanya hivyo tena kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambapo alifunga bao la kwanza kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC.

Tanzania, Zambia zasaini mikataba nane ya ushirikiano
Jaribio la kwanza kwa kocha Zuberi Katwila