Mara baada ya Serikali kukamilisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa sheria mpya ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma ya mwaka 2018 imetangazwa sheria hizo kuanza rasmi utekelezaji wake leo Agosti 1, 2018.
Sheria hiyo mpya ni ile inayounganisha mifuko ya pension minne ya PSPF, LAPF PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja wa PSSSF ambapo sasa kutakuwa na mifuko miwili ya hifadhi ya jamii wa Shirika la taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) na mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF).
Hayo yameelezwa na Waziri, wa nchi ofisi ya waziri mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenister Mhagama akiwa Jijini Dodoma.
Hatua hiyo ni kufuatia uamuzi uliofikiwa JanuarI 31 mwaka huu na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kupitisha sheria mpya ya mfuko wa hifadhi ya watumishi wa umma (The Public Service Social Security Fund Act No.2 of 2018) pamoja na mambo mengine ambapo sheria hiyo inaunganisha mifuko minne ya pension ya PSPF,LAPF PPF na GEPF na kuwa mfuko mmoja unaoitwa Mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma (PSSSF).
Sheria hiyo pia imefanya marekebisho kwenye sheria ya shirika la taifa la hifadhi ya jamii NSSF ili kufanya mfuko huo kuhudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta zisizo rasmi.