Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amewasili Mjini Entebbe nchini Uganda kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia tarehe 23 Novemba 2021 mpaka tarehe 26 Novemba 2021 ambapo atapata fursa ya kujifunza mafanikio ya Kilimo bora cha Michikichi.
Katika ziara hiyo Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye, Mkurugenzi wa Maendeleo Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu na wataalam wengine wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Waziri Mkenda atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda Mhe. Frank Kagyigyi Tumwebaze, kadhalika atafanya ziara kwenye kiwanda cha kampuni ya Wilmar International ambayo imeonyesha nia kuwekeza kiwanda cha mafuta ya kula kwa ubora wa mwisho kutokana na uzalishaji wa michikichi, alizeti na maharage ya soya nchini Tanzania.
Waziri Mkenda amesema kuwa ili uwekezaji huo uwe na tija uhakika wa malighafi ni suala muhimu ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo bora wa uzalisaji kama vile mashamba makubwa (Block Farming) yanayowahusisha wakulima wadogo.
Amebainisha kuwa kwa upande wa Michikichi kampuni hiyo ingependa kuanzisha mashamba ya pamoja yenye ukubwa wa angalau ekari 10,000 kwa kila shamba.