Serikali imesitisha bei mpya ya mafuta ya petroli na dizeli iliyotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Mafuta na Maji (EWURA) ambazo zilitarajiwa kuanza Septemba 1 mwaka huu na kuagiza tume ifanye uchunguzi kuhusu bei hizo.
Hayo yamesemwa na Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa leo Septemba 4, 2021 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma ambapo amesema kuwa bei ya zamani itaendelea.
“Kulitokea taarifa mbili, kwanza EWURA walitoa bei mpya za mafuta kuanzia Septemba 1, baadaye wakasitisha. Waziri Mkuu aliliona hilo akaagiza bei hizo mpya ziangaliwe upya, lakini bei za awali zikute zinaedelea. Kwa hiyo sasa hivi zinaendelea bei za mwezi Agosti”.amesema Msigwa
“Kamati aliyoagiza Waziri Mkuu kuchunguza suala la bei ya mafuta tayari imeanza kazi, itatoa ripoti baada ya wiki mbili. Wataangalia mfumo wa ukokotoaji wa bei, utaratibu wa ununuzi wa mafuta, tozo, kampuni zinazoagiza mafuta nje na utaratibu uliowekwa bandarini”.amesema Msigwa
“Lengo ni kujua sababu za kupanda kwa mafuta na kujua kama kuna maeneo yanayoweza kushughulikiwa ili Watanzania waendelee kupata mafuta kwa bei nafuu, kwani kupanda kwa bei ya mafuta kuna madhara katika uchumi,” amesema Msigwa.