Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ikiimarishe kituo cha utafiti wa zao la michikichi cha Kihinga kilichopo mkoani Kigoma kwa kukitengea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu pamoja na barabara ili kuboresha shughuli za utafiti zinazofanywa kituoni hapo.

Aidha, ameitaka wizara hiyo ihakikishe suala la utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu zao la michikichi linaimarishwa na kupewa kipaumbele, na kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuhakikisha utafiti wa mbegu unaofanywa una tija.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wadau wa zao la michikichi katika ukumbi wa NSSF, Kigoma ambapo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kuwekeza katika zao hilo ili kujiongezea kipato.

“Wizara ya Kilimo hakikisheni mnatumia vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa zao la michikichi. Pia tumieni magari maalumu kwa ajili ya kutolea elimu kwa umma kuhusu zao la michikichi na faida zake.”

Waziri Mkuu amesema hadi sasa mbegu zilizozalishwa tangu kuanza kwa zoezi hilo ni 4,205,335 ambazo zinatosha kupanda eneo la ekari 84,106.7, kati yake asilimia 71 imechangiwa na Wizara ya Kilimo kupitia TARI na asilimia 29 ni mchango wa sekta binafsi (FELISA & Ndugu Development Foundation (NDF) na Yangumacho Group).

Mpaka sasa mbegu 2,184,111 zimeshasambazwa na TARI kwa ajili ya kuziotesha ili miche bora iweze kusambazwa kwa wakulima na kati ya mbegu zinazooteshwa tayari miche 1,370,318, imeshaota na kupandwa kwenye viriba vidogo na vikubwa ikiwa ni hatua ya kuzifikisha kwa wakulima.

Mahitaji ya mafuta nchini kwa sasa ni zaidi ya tani 570,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 210,000 tu, hivyo, kiasi cha tani 360,000 huagizwa kutoka nje ya nchi na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 443 kila mwaka.

EAC yaipongeza Tanzania kwa Miradi ya Kimkakati
Trump akinzana na waziri wake wa mambo ya kigeni

Comments

comments