Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amechangia mifuko 300 ya saruji na fedha sh. milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) la Magomeni, Mwembechai, jijini Dar es Salaam.
Majaliwa ametoa mchango huo leo Mei 11, 2019 kwenye sherehe za kutimiza miaka 100 ya Idara ya Huduma za Familia ya Kanisa la Sabato Ulimwenguni zilizofanyika kwenye kanisa hilo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini wa makanisa mbalimbali ya kanisa la SDA waliohudhuria sherehe hizo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango unaotolewa na taasisi za dini na akalishukuru kanisa la SDA kwa kuamua kutoa huduma za elimu, afya na maji bila ubaguzi wowote wa dini.
“Mbali na kutoa huduma za kijamii, kanisa hili pia linamiliki vyombo vya habari vya Morning Star Radio FM, Adventist World Radio (AWR) na Hope Channel Tanzania TV ambavyo hutoa elimu kwa watu mbalimbali. Kupitia elimu mnayotoa, mmesaidia watu wote kwa maisha ya sasa na ya baadaye,” amesema.
Ametoa wito kwa maaskofu na wachungaji waendelee kuhimiza waumini wao wafanye kazi kwa bidii ili kuendana na maono ya kanisa hilo yanayotaka watu wafanya kazi, watoe sadak a na zaka na kisha walipe kodi.
“Maaskofu na wachongaji mundelee kuhamasisha utendaji kazi kwa Watanzania wote. Pia muwahamasishe vijana wajiunge kwenye vikundi na kubuni miradi ya kujiletea maendeleo kwani Serikali haiwezi kutoa ajira kwa wahitimu wote,” amesema.
“Wahimizeni pia vijana wajifunze stadi za kazi ili waweze kupata ujuzi. Na Serikali hii tunahimiza ujenzi wa viwanda, kwa hiyo tunahitaji vijana wenye ujuzi ili kuendana na kauli ya Serikali isemayo Tanzania ya Viwanda ifikapo mwaka 2025.”
Amewapongeza viongozi wa kanisa kwa kuamua kutafsiri kitabu cha Tumaini kwa Familia za Leo ambacho kinalenga kuhuisha mahusiano katika familia. “Nimesikia mahubiri yakihimiza mahusiano baina ya wanandoa na baina ya wazazi na watoto. Nakubaliana na mafundisho ya Baba Askofu kwamba Taifa imara siku zote, msingi wake ni familia imara. Ni vema kila Mtanzania akasoma kitabu hiki. Kila mmoja apate nakala ikiwemo Waislamu na Wakristo wa madhehebu mengine.”
Naye Askofu SDA Jimbo la Kusini, Mch. Mark Malekana amesema Mungu aliandaa ndoa ili iwe mahali pa furaha, amani, upendo na maelewano lakini kwa sasa shetani ameamua kuharibu mpango wa Mungu kwa kuweka migogoro baina ya wanandoa.
Amesema kanisa la SDA liliamua kuwa na idara ya familia lengo kuu likiwa ni kuzirudisha ndoa kwenye kusudi la Mungu. Mwenza wako ameumbwa awe ni wa kufaana nawe, siyo kufanana na wewe. Kama unadhani mke wako kufikiri tofauti na wewe ni tatizo, kuabnzia leo futa hiyo dhana. Mmeumbwa tofauti ili mmsaidiane kusinga mbele,” alisema.
“Matokeo ya migogoro ya kwenye ndoa ni kuongezeka kwa watoto wa mitaani; tembea kokote kule hapa nchini au nje ya nchi utabaini kuwa hii ni tatizo kubwa. Wanandoa tutimize wajibu wetu kwa malezi ya familia ili ndoa zetu zirudi Eden,” alisisitiza.
Akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa Jimbo la Kusini, Mch, Dkt. Rabson Nkoko alisema kanisa hilo linatoa huduma za elimu, uchapishaji, afya, vyombo vya habari, maafa na kwenye maendeleo.
“Kanisa linamiliki taasisi ya Adventist Development and Relief Agency (ADRA) ambayo mwaka 2018 ilitoa misaada yenye thamani ya dola za Marekani 89,031 (sawa na sh. milioni 204.77) kwa watu 18, 332 katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu; watu waliopatwa na mafuriko Meru na Arusha; na watu wenye ulemavu wa ngozi nchini na maeneo mengine,” alisema Mch. Nkoko.