Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaalika wafanyabiashara kutoka Korea Kusini waanzishe miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani.
Majaliwa ametoa mwaliko huo leo Julai 23, 2018 akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon wakati akifungua Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Korea lililofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kongamano la kwanza lilifanyika jijini Seoul, Februari 2018.
Amesema Serikali inahamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vinavyotumia rasilimali za ndani ambavyo vitasaidia kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo, misitu, madini na bahari.
“Tunakaribisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo ya uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za walaji (consumer goods), pamoja na viwanda vya kuunganisha bidhaa mbalimbali, yaani (assembling plants) kama vile magari, simu na majokofu,” amesema.
Waziri Mkuu pia aliwaalika wafanyabiashara kutoka Korea waliohudhuria kongamano hilo waje kuwekeza kwenye sekta ya utalii ambako alisema kuna vivutio vya mbuga za wanyama kama Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Olduvai Gorge na fukwe za bahari za Tanzania bara na Zanzibar.
“Tanzania ina kilometa 1,200 za fukwe kuanzia Tanga hadi Mtwara, ziko pia fukwe za Zanzibar, ziko fukwe kwenye maziwa yetu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ambazo ni kivutio kingine cha utalii,” amesema.
Amesema ili kusimamia matumizi ya fukwe hizo, Serikali inakamilisha uundaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Fukwe kama ilivyo ile ya Ngorongoro ambayo alisema taratibu zikikamilika, itaanza kazi hivi karibuni.
Naye, Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-yon amewapongeza viongozi wa Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mageuzi ya kiuchumi hadi kuiwezesha nchi hii kuwa mojawapo ya nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa haraka.
“Mapema mwaka huu, Benki ya Dunia imeitambua Tanzania na kuitangaza kuwa ni miongoni mwa nchi 10 ambazo uchumi wake unakua kwa haraka duniani. Nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Serikali hii pamoja na wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchi hii,” alisema.
Ametumia fursa hiyo kuwaeleza wafanyabiashara na wenye makampuni kutoka Korea ambao wanashiriki kongamano hilo kwamba amepokea maombi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ambaye ameyaalika makampuni ya Kikorea yashiriki kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji.
“Ukiondoa mradi wa ujenzi wa daraja la Salender ambao mkataba wake umesainiwa leo, Rais Magufuli ameomba makampuni ya Kikorea yashiriki kwenye miradi mikubwa ya kiuchumi na hivi karibuni, taratibu zikikamilika, kuna kampuni moja itasaini mkataba wa kujenga meli kubwa kwenye Ziwa Victoria, na siyo huko tu, hata kwenye Ziwa Tanganyika,” alisema.
Waziri Mkuu wa Korea Kusini ameondoka nchini leo jioni Julai 23, 2018.