Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka vijana wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi waache kukaa vijiweni na badala yake waanzishe bustani ili kujiongezea kipato.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Julai 18, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.
“Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime, twende shambani. Shamba siyo lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama muhogo. Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana.”
Amesema Serikali imetoa sh. milioni 600 ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji huko Mpumbe, Mnindu, Chiepo na Chikalala. “Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime wakati wote, iwe masika au kiangazi. Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia kipato zaidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kamati ya ujenzi ya mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu wa ujenzi wa majengo ya Serikali kwenye soko hilo.
Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Bw. Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch) badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.
Pia alimwagiza Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Bw. Harun Ibrahim Kiara ahakikishe wanatoa elimu ya kilimo cha bustani kwa vijana ili waanze na matuta machache. “Pia anzisheni programu ya kukutana na vijana na akinamama na muwaeleze bonde la Mnindu linatumikaje kwa kilimo hicho,” amesema.