Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasili nchini Tunisia akitarajiwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD, ambao unaanza hii leo Jumamosi, Agosti 27, 2022.
Majaliwa aliwasili nchini humo (Ijumaa Agosti 26, 2022) na na kupokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najla Bouden Romdhane katika uwanja wa ndege wa Carthage, jijini Tunis.
wakiwa uwanjani hapo, wawili hao walipata wasaa wa kubadilishana mawazo na mwenyeji wake na walijadiliana masuala kadhaa kuhusu demokrasia na utawala bora, uhusiano wa kimataifa na uchumi.
Mkutano huo utakaofanyika Agosti 27-28, 2022 unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na ajenda za kimaendeleo zitakazotekelezwa kati ya Japan na Afrika ambapo Rais wa Senegal, Macky Sall na Waziri Mkuu wa Japan, Kishida Fumio watatoa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.
Tanzania imekuwa ikishiriki mikutano hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993, kufuatia mahusiano mazuri kati yake na Japan kupitia Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo (JICA), unaotekeleza miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, maji, elimu, afya na kilimo.