Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Julai 19, ametoa taarifa ya miamala ya simu na kusema kuwa, serikali imesikia kilio cha wananchi na inaendelea kuyafanyia kazi, ambapo Waziri mkuu ameitisha kikao kesho Julai 20.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa kwa sababu hii ni sheria ya Bunge, na tayari imeshapitishwa na inatakiwa kutekelezwa, lakini kuna maeneo ambayo yanaangukia kwenye kanuni ambazo zinaangukia Wizara ya Fedha na Wizara ya Teknolojia ya Mawasiliano.
“Nitoe rai kwa wananchi kuwa Serikali imesikia malalamiko ya wananchi na tayari tumeendelea kuyafanyia kazi, Waziri Mkuu ameshaitisha kikao kesho kuendelea kupitia masuala haya haya.” amesema Waziri Nchemba
“Nitoe rai kwa ambao wanapenda kupotosha au kubadili dhana ya jambo ambalo limekusudiwa la lina maslahi mapana ya Taifa letu wasifanye hivyo. Sheria za nchi zinapaswa ziheshimiwe, hakuna haja ya kuwasikiliza wapotoshaji”
“Tumeshawaelekeza wataalam wetu waangalie kipengele kinachozungumzia masuala ya National Payment System ambayo inaongelea masuala ya miamala na Electronic and Postal Communication. Timu za wataalam pamoja na sisi tutaendelea kuyafanyia kazi.
Amesema, Tuendelee kumuunga mkono Rais Samia katika ujenzi wa taifa letu ili tuweze kuwakomboa Watanzania na kuleta maendeleo endelevu katika Taifa letu.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amewasihi watanzania tuwe watulivu wakati jambo hili linafanyiwa kazi, Serikali yetu ni sikivu, na itaenda kulifanyia kazi jambo hili kuhakikisha tunafikia mwafaka mzuri.
“Sisi kama Wizara, tumeguswa na hili, tumekuwa tukikusanya maoni, ushauri na kuchakata takwimu tangu tozo hii ianzishwe, nikuhakikishie Wizara yangu itakupa ushirikiano Mhe. Waziri (Mwigulu) ili maelekezo ambayo tumepewa tufikie hatua nzuri,” amesema Dk. Ndugulile.