Mkazi wa Kijiji cha Kabanga wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Leonard Nkamba anayejishughulisha na uchongaji wa vyombo mbalimbali vya jikoni ameishukuru Serikali kwa kuanzisha sera ya viwanda kwa kuwa imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ameyasema hayo baada ya kukabidhiwa kiasi cha sh. milioni 2.5 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili aweze kuongeza mashine itakayomuwezesha kuchonga bidhaa zenye ubora zaidi.
Bidhaa anazochonga ni vikombe, chupa za chai, hotpot kwa kutumia mti aina ya jakalanda, ambapo pia anachonga vibao na kuandika ujumbe mbalimbali kwa kutumia unga wa ngano.
Amesema kuwa anaushukuru Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao uliona kazi zake na kumuagiza atengeneze seti za vyombo kwa ajili ya zawadi za kumpelekea Rais Dkt. John Magufuli.
“Uongozi wa UWT mkoa wa Kigoma na Taifa ulivutiwa na kazi zangu na kuniagiza nitengeneze chupa ya chai, vikombe na hot pot kwaajili ya kumpa zawadi Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu ndipo Waziri Mkuu jana aliona kazi zangu na akavutiwa na bidhaa ninazotengeneza ndipo akaniuliza kama kuna changamoto zinazonikabili, nikamwambia nahitaji mashine moja yenye thamani ya sh. milioni mbili na nusu akasema umepata na leo sijaamini alivyoniita na kunikabidhi. Namshukuru sana.”amesema Nkamba
Aidha, Nkamata ametumia fursa hiyo kuwashauri wananchi wengine hususani vijana kuacha kulalamikia suala la ukosefu wa ajira na badala yake wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali na kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo wataziuza na kujipatia kipato.
Pia amewaomba Watanzania wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vya ndani kwa kuwa vina ubora wa kutosha na pia watakuwa wanachangia kukuza uchumi wa wajasiriamali na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili waweze kujipatia kipato na kuondokana na umasikini, pia amesema Serikali ipo tayari wakati wowote watakapohitaji msaada.
Waziri Mkuu amempongeza mjasiriamali huyo kwa bidhaa mbalimbali anazotengeneza ambazo ni nzuri na za kipekee. ambapo amesemma kuwa amefurahi kuona vikombe, chupa za chai pamoja na hot pot zilizotengenezwa na Mtanzania kwa kutumia miti.