Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Meneja wa wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Morogoro, mhandisi Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja baada ya kuzembea katika kutimiza majukumu yake.
Ameutoa uamuzi huo baada ya Mhandisi Andalwisye kushindwa kufanya ukaguzi wa usalama wa madaraja yaliyoko kwenye mkoa wake na kubaini kama kuna daraja lina matatizo, hali iliyosababisha daraja la Kiyegea lililopo eneo la Gairo ambalo linaunganisha mkoa wa Morogoro na Dodoma kuvunjika.
Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ukarabati unaoendelea kwa lengo la kurejesha mawasiliano ya barabara.
“Hivi unajua udhaifu wako ni kwa sababu hukufanya ukaguzi kuona kama daraja limejaa mchanga au uchafu ambao umesababisha kipenyo cha kupitisha maji kuwa kidogo na maji yakalazimika kupanda juu hali ambayo ilisababisha daraja hili kusombwa na maji,” amehoji Waziri Mkuu.
Ameelekeza wakati njia hiyo inarekebishwa itengenezwe njia nyingine ya muda ili kuweza kupitisha magari na kisha serikali itachukua hatua baada ya kubaini nini kimesababisha.
Ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa haraka, Waziri Mkuu ameagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, Katibu Mkuu wa wizara hiyo pamoja na Wahandisi wote wa TANROADS mkoa wa Morogoro na Dodoma wakutane kwenye eneo la tukio na wahakikishe kuanzia njia hiyo imefunguka.