Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Khadhimi, amenusurika jaribio la mauaji lililofanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani zenye silaha zilizoyalenga makaazi yake katika Ukanda wa Kijani wenye ulinzi mkali mjini Baghdad.
Maafisa wa serikali yake wamesema Khadhimi hakudhurika kutokana na mashambulizi hayo yaliyofanika mapema siku ya Jumapili Novemba 7.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, Maafisa wawili wa serikali ya Iraq waliliambia shirika hilo kuwa walinzi saba wa Khadhimi walijeruhiwa kwa mashambulizi ya ndege mbili zenye silaha zisizo rubani, yaliyotokea kwenye eneo mashuhuri la Ukanda wa Kijani, ambalo kawaida linakuwa na ulinzi mkali.
Taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali ilisema jaribio hilo lililoshindwa la mauaji lilifanyika “kwa ndege yenye miripuko ambayo ilijaribu kuyapiga makaazi ya waziri mkuu katika Ukanda wa Kijani.”
“Vyombo vya usalama vinachukuwa hatua zinazohitajika kuhusiana na umuhimu na jaribio hili lililoshindwa,” ilisema taarifa hiyo.
Haikufahamika mara moja aliyehusika na mashambulizi hayo wala hakukuwa na aliyebeba dhamana yake, lakini yametokea wakati kukiwa na mkwamo baina ya vikosi vya usalama na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, ambao wafuasi wao wamepiga kambi nje ya Ukanda wa Kijani kwa takribani mwezi mzima baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa bunge, ambao walishindwa vibaya.
“Jaribio hili la mauaji ni kiwango cha juu cha kuzorota kwa hali, yakivuuka mpaka katika njia isiyotegemewa ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kabisa,” aliandika Ranj Alaadin, mtaalamu wa Taasisi ya Brookings katika ukurasa wa Twitter.