Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vyumba viwili vya madarasa vikiwa na madawati vyenye thamani ya sh. milioni 80 kutoka kwa bank ya CRDB.
Majaliwa amepokea msaada huo katika shule ya Sekondari Kassim Majaliwa iliyopo Kata ya Nachingwea katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi
Amewashukuru uongozi wa benki ya CRDB kwa msaada hu ambao umesaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa unaoikabili wilaya hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu alizitaka taasisi nyingine ziige mfano wa bank ya CRDB kwani imekuwa bega kwa bega na Serikali katika kuchangia shughuli za kimaendeleo nchini.
Pia, ametoa wito kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kassim Majaliwa kutumia vizuri madarasa hayo na kutunza mali zilizopo shuleni hapo.
Amesema ujenzi wa shule hiyo ni mradi uliobuniwa na wakazi wa kata ya Nachingwea ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu katika eneo lililo karibu na makazi yao.
“Nawaomba wananchi wenzangu tuendelee kushirikiana katika kuibua na kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo kwenye kata yetu ya Nachingwea.”
Pia Waziri Mkuu alikabidhi kompyuta 20 kwa shule za sekondari tano ambazo ni Kassim Majaliwa, Likunja, Mnacho, Hawa Mchopa na Ruangwa.