Shambulio la anga, lililofanywa na ndege za Serikali katika eneo la Mekele lililopo Mkoa wa Tigray limesababisha vifo na majeruhi ambao idadi yake bado haijafahamika, huku Waziri Mkuu, Abiy Ahmed akishutumiwa kwa uharibifu ulitokea Chuo kikuu cha Mekele.
Msemaji wa waasi wa Tigray na afisa wa hospitali ya Mekele, Getachew Reda amesema shambulio hilo linakuja ikiwa ni siku ya tatu baada ya waasi wa Tigray kusema wako tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika (AU).
Amesema, mazungumzo hayo yalipangwa kusimamiwa na AU kati ya waasi hao wa Tigray na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed baada ya vita ambavyo vimekuwa vikiendelea tangu Novemba 2020 na sasa shambulio hilo linaweza kuleta ukakasi katika hatua hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hospitali Mkoa wa Tigray, Kibrom Gebreselassie naye kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kuwa Mekele ilishambuliwa na ndege zisizo na rubani mapema leo asubuhi, mtu mmoja aliyejeruhiwa amefika katika hospitali ya Ayder na dadi kamili ya waathiriwa bado haijajulikana.”
Mapigano kaskazini mwa Ethiopia yamekuwa yakifanyika kutokana na kuanza kwa uhasama baada ya makubaliano ya miezi mitano Agosti 24, 2022 na pande zote mbili zimekuwa zikilaumiana kwa kuanzisha mashambulizi ambayo huleta madhara.
Waasi hao, wamekuwa wakiyashutumu majeshi ya Ethiopia na Eritrea kwa kuanzisha mashambulizi ya pamoja kutoka Eritrea, ambayo inapakana na Tigray kaskazini, na kudai hapo awali ilisaidia vikosi vya Ethiopia katika awamu ya kwanza ya mzozo huo.