Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amezindua rasmi jengo la Bodi ya Mkonge Tanzania (Mkonge House) lililoko Jijini Tanga ambalo lilikuwa ni moja ya mali zilizorudishwa na Serikali kwa wananchi na wakulima wa mkonge.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu amesema Tanzania ni moja ya nchi ambayo ilikuwa mzalishaji mzuri wa zao hilo katika kipindi cha miaka 60 iliyopita ambapo ilikuwa inazalisha tani zaidi ya 235,000 ikiwa ni nchi ya kwanza duniani.
“Zao hili miaka 60 iliyopita Tanzania ndiyo ilikuwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa mkonge tani zaidi ya 235,000 na zao hili lilikuwa linatuletea fedha nyingi za kigeni zaidi ya asilimia 65, lakini lilishuka katika uzalishaji mpaka tani 36,000, kwa hiyo Serikali imechukua hatua kubwa kurudisha heshima ya zao la mkonge”. Amebainisha Majaliwa
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeweka Mkakati wa kurudisha na kuimarisha mazao muhimu ya kimkakati ambayo ni pamoja na pamba, kahawa, tumbaku, korosho, alizeti na sasa imeongeza zao la mchikichi na mkonge ili kuwawezesha wakulima kuwa na uwanda mpana wa kuinua uchumi wao.
Ametoa agizo kwa Mamlaka za Mikoa kuwasaidia wananchi wanaotaka kulima zao hilo kupitia ushauri na hamasa kutoka kwa Maafisa kilimo ili kuwezesha uzalishaji wenye tija.
“Kila mkoa, kwa mwananchi anayetaka kulima zao la mkonge Serikali kupitia mikoa hiyo iwasaidie wakulima wote, wadogo wenye uwezo wa kulima hekari moja, wakulima wa kati kuanzia hekari 5-15 na wakulima wakubwa kuanzia hekari 15 wapewe uwezeshaji ili walime na wapate faida kubwa, mkonge ni fedha kwa hiyo wananchi limeni kwa manufaa”. Amesema Waziri Mkuu.
Aidha ameitaka Bodi mpya iliyoithibitishwa leo kuwa Bodi rasmi ya Mkonge kutumia fursa ya vyombo vya habari kuwahabarisha wananchi namna ya kulima mkonge, faida, fursa za zao hilo na kuwapa hamasa wakulima hao kuzalisha zao hilo katika mikoa inayolima ikiwemo Tanga, Morogoro, Pwani, Kilimanjaro na Mkoa wa Shinyanga.