Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uhakikishe kuwa vijana wote wanaomaliza darasa la saba kwenye kila Halmashuri za mkoa huo wanakwenda kuanza kidato cha kwanza.
Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili kwenye uwanja ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma.
Amesema kuwa Halmashuri zote za mkoa huo zijikite katika kujenga madarasa ili wanafunzi wote waliofaulu ambao wanatakiwa kwenda sekondari waende.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuahakikisha kwamba watoto wote wenye sifa za kupata elimu ya seondari wanapata elimu hiyo kote nchini hivyo juhudi za makusudi lazima zifanywe na kila Halmashauri ili kutimiza azma.
Akizungumzia suala la utoro shuleni, Waziri Mkuu amesema hilo ni moja kati ya maeneo yanayozorotesha juhudi kubwa za Serikali za kuwapatia watoto wa Tanzania elimu katika maeneo mengi nchini na lazima viongozi wa wilaya na mikoa wasimame imara ili kukomesha hali hiyo.
Amesema viongozi wa ngazi zote katika mikoa na wilaya ndiyo hasa wanaoweza kumaliza tatizo la utoro wakishirikiana kwa karibu na wanavijiji ambao wanaishi na watoto hao na wanajua ni watoto wangapi hawaendi shule.
Hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kutoa maelekezo na miongozo itakayowabana watoto watoro pamoja na wazazi au walezi wao kwani wanayo mamlaka na uwezo wa kuchukuwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.