Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa siku 21 kwa viwanda vyote nchini vinavyozalisha vileo viwe vimefunga mfumo ukusanyaji kodi kwa kutumia stempu za kielektroniki.
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akiahirisha mkutano wa kumi na nne wa Bunge la kumi na moja, Bungeni jijini Dodoma leo Februari 9, 2019.
Majaliwa pia ameziagiza Wizara na Taasisi zote za Umma ziwe zimejiunga na Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (GePG) kabla ya Juni mwaka huu.
Amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isimamie uwekaji wa mifumo hiyo na ifikapo februari 28, 2019 kila kiwanda kiwe kimefunga mfumo huo.
“Naielekeza TRA kusimamia uwekaji wa mifumo ya kukusanya kodi za vileo kwa kutumia stempu za kielektroniki kwa viwanda vyote vinavyozalisha vinywaji hivyo.”
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha na rasilimali za umma ili kufikia malengo.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutumia mfumo wa kielektroniki wa stempu za kodi kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na zile zinazoingizwa nchini.
Amesema mfumo huo utasaidia Serikali katika kupata taarifa sahihi za uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato ya Serikali.