Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumkumbuka Augustino Lyatonga Mrema kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza mahusiano na vyama vya siasa nchini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo hii leo Jumatano, Agosti 24, 2022, wakati akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga marehemu Mrema katika Parokia ya Mt. Augustino Kilimahewa, Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema, “Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa.”
Waziri Mkuu amefafanua kuwa, “Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa Serikali na upande wa siasa lakini pili, tuendelee kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema peponi.”
Kuhusu mazishi ya Mrema, ambayo yanayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi ya Agosti 25, 2022 Kiraracha Moshi, Waziri Mkuu amesema Serikali itawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
Akizungumza na niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi hilo, DCP Anthony Luta amesema Jeshi la Polisi litaendelea kumkumbuka Mrema kwa hatua yake ya kuanzisha jeshi la ulinzi wa sungusungu, ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na utetezi wa haki za wanawake ambapo kwa sasa wameanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi.
Naye, Paroko wa kanisa hilo Padre Peter Assenga amesema Mrema alikuwa akijitolea kwa mambo mengi parokiani hapo huku Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akisema umati uliopo kanisani hapo ni ishara tosha ya jinsi Mrema alivyoishi vizuri na watu wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.
Ibada hiyo, iliongozwa na Askofu mmoja na mapadre sita, huku baadhi ya viongozi waliohudhuria wakiwa ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Hamad Rashid, Prof. Ibrahim Lipumba, John Cheyo, Steven Wassira, James Mbatia, Joseph Selasini na Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro.
Katika msiba huo, salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ziliwasilishwa mapema hii leo asubuhi na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ambaye alifika hapo kuwapa pole ndugu jamaa na marafiki wa Marehemu Mrema.