Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu unaojengwa na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na amezitaka wilaya nyingine kuiga mfano huo.
Uwanja huo unaoitwa Majaliwa umezinduliwa kwa mechi kati ya timu ya wilaya ya Ruangwa ya Namungo FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza na timu ya Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo ndio mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, 2018/2019.
Waziri Mkuu amezindua uwanja huo leo (Jumamosi, Agosti 11, 2018), ambapo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa na wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi huo.
Uwanja huo unajengwa katika kitongoji cha Mtichi kata ya Nachingwea na ndio utakaokuwa unatumiwa na timu ya Namungo FC kuchezea mechi za nyumbani.
Amesema suala la ujenzi wa uwanja ni jambo muhimu na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linahamasisha ujenzi wa uviwanja katika ngazi za mikoa na wilaya ili kutoa fursa kwa wananchi hususani vijana kushiriki katika michezo, hivyo amezitaka halmashauri nyingine ziige mfano wa wilaya ya Ruangwa.
Akizungumzia kuhusu mechi ya kirafiki kati ya timu za Simba na Namungo, Waziri Mkuu amesema “Michezo ni burudani na wananchi wanataka kuburudika, Simba chapeni kazi onesheni uwezo wenu wa mwisho ili Namungo nao waweze kupata ufundi,”.
Pia amesema mbali na kucheza na Simba, timu hiyo ya Namungo inatarajiwa kucheza na timu ya Dodoma FC ya jijini Dodoma keshokutwa (Jumatatu, Agosti 13, 2018). Pia timu hiyo itacheza na timu za Yanga na Azam za jijini Dar es Salaa hivi karibuni.
Waziri Mkuu ametaja faida ya timu kama za Simba, Yanga, Azam na Dodoma FC kucheza na timu ya Namungo FC kuwa ni pamoja na kuwaimarisha wachezaji kwa kuwafanya wajiamini na kuondoa uoga wa kupambana na timu nyingine.
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza timu ya Namungo FC kwa hatua waliyofikia, kwani ilianza kwa kushiriki mashindano ya kugombea kuku, mbuzi na ng’ombe na sasa inashiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara. “Hakikisheni mnafikia lengo letu la kucheza ligi kuu,”.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi amesema kutokana na jitihahada za kuboresha maendeleo zinazofanywa na Mbunge wa jimbo la Ruangwa ambaye ndiye Waziri Mkuu, uongozi wa mkoa umeamua kuupa uwanja huo jina la Majaliwa ili kumuenzi.
Kwa upande wake, Msemaji wa Timu ya Simba, Bw. Haji Manara amesema timu hiyo ipo Ruangwa na benchi lake lote la ufundi wakiwemo wachezaji 27 na kwamba ameshangazwa na wingi wa watu waliojaa uwanjani hapo.
“Hakuna uwanja Tanzania unaoweza kujaza watu 20,000 kwa mechi za kawaida nje ya Dar es Salaam na Mwanza. Nimeambiwa kulikuwa na tiketi 20,000 ambazo zimeisha zote,” amesema.