Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutafakari namna ya kurekebisha baadhi ya dosari zilizopo likiwemo suala la kuwanyima mikopo wanafunzi kwa kutumia kigezo cha kusoma katika shule binafsi.

Amesema kuwa kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamefaulu vizuri kidato cha nne na wamekosa nafasi katika shule za Serikali na wanatoka katika familia zisizokuwa na uwezo, hivyo wanatafuta wafadhili ambao wanawasomesha kwenye shule binafsi.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Agosti 10, 2019) wakati akifungua mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema kitendo cha bodi hiyo kuwanyima mikopo baadhi ya wanafunzi kwa kigezo cha kusoma katika shule binafsi bila ya kujiridhisha kama wanatoka kwenye familia zenye uwezo au zisizokuwa na uwezo kinawanyima wanafunzi hao fursa za kuendelea na masomo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa vyuo vikuu kuimarisha mafunzo kwa njia ya vitendo kwani tafiti nyingi zinazohusu mambo ya ajira zimebainisha umuhimu wa mafunzo ya vitendo katika kumuwezesha mhitimu kuwa na uelewa na ujuzi mpana wa kile alichokisoma kwa njia ya nadharia.

“Vyuo viongeze umakini na ufuatiliaji wa karibu wa vijana wetu wanapokuwa kwenye elimu kwa vitendo ili kuhakikisha kwamba wanapata maarifa na ujuzi uliokusudiwa katika mitaala yao. Pia natoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi watoe ushirikiano wa dhati kwa wanafunzi wanaotafuta nafasi za kufanya mafunzo kwa njia ya vitendo kwenye taasisi zao.”amesema Majaliwa

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO, Peter Niboye amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu ni ucheleweshwaji wa mikopo kwa baadhi ya vyuo licha ya HESLB kuwasilisha fedha hizo mapema, hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia katika kutatua tatizo hilo.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo wa TAHLISO, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa ushirikiano mkubwa inaoipatia jumuiya hiyo hivyo kurahisisha utendaji wake.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amemkabidhi Waziri Mkuu hati ya kiwanja kilichoko katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TAHLISO, ambapo baada ya kupokea hati hiyo, Waziri Mkuu aliikabidhi kwa Mkwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa Niboye.

Mkutano huo umehudhuriwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godfrey Chongolo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori pamoja na viongozi kutoka vyuo mbalimbali nchini vinavyounda TAHLISO.

Jeshi la Polisi latoa idadi kamili ya waliofariki kwenye ajali ya Lori Morogoro
JPM atuma salamu za rambirambi ajali ya Morogoro