Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajia kuanza ziara ya kukiombea kura chama chake mkoani Kagera ambapo atafanya mikutano mbalimbali ya hadhara.
Akiongea na waandishi wa habari mjini Bukoba,katibu mwenezi wa chama hicho mkoani Kagera Hamimu Mahamudu amesema kuwa chama chao kinaendelea na kampeni za kuomba kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao hivyo kiongozi huyo ataanzia kampeni zake wilaya ya Bukoba.
“Kama tunavyojua ndugu wanahabari waziri mkuu ni mlezi wa mkoa wetu kichama hivyo kesho ataanza kampeni kama ilivyo ada atafanya mikutano akianzia Rubale halmashauri ya wilaya Bukoba na baadaye jioni atakuwa na mkutano mwingine wa hadhara uwanja wa mayunga Manispaa ya Bukoba,” amesema Hamimu.
Hamimu ameongeza kuwa Majaliwa atakuwa na ratiba ya siku tatu katika mkoa huo ambapo atakwenda pia Kyerwa,Missenyi, Karagwe Ngara na baadaye kumalizia Biharamulo wakati akielekea mkoani Geita ambapo amewaomba wananchi kujitokeza hasa katika maeneo ya mikutano.
Aidha amewaomba wananchi wa mkoa wa Kagera kuwa nje ya mikutano ya hadhara waziri mkuu atafanya mikutano ya njiani ya kuomba kura katika maeneo mbalimbali hivyo wananchi watakao kuwa katika maeneo ya njiani ambapo atapita wajitokeze kuja kumsikiliza.
Waziri Mkuu akiwa Kagera atafanya mkutano Issingilo kwa upande wa Kyerwa, Bunazi uwanja wa mashujaa kwa wilaya ya Missenyi, Kayanga Karagwe uwanja wa Changalawe na mjini Ngara pamoja na Nyakanazi kwa wilaya ya Biharamulo.