Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza mamia ya watu wenye ulemavu kwenye matembezi ya hiari kumuenzi muasisi wa Taasisi ya dkt. Regnald Mengi kwa watu wenye ulemavu (DRMF), kuhitimisha mwezi wa kumbukizi ya matendo ya huruma aliyoyafanya dkt. Mendi enzi za uhai wake.
Matembezi hayo yanatarajiwa kufanyika Mei 31, mwaka huu kwa kuhitimisha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kupanda miti kulinda vyanzo vya maji, kuchangia damu na michezo jumuishi kwa wenye ulemavu zitakazo anza kufanyika Mei Mosi mwaka huu.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Shimimana Ntuyabaliwa amebainisha kwamba Mei ni mwezi wenye matukio matatu muhimu kwa dkt. Mengi hivyo lazima kufanya mambo aliyoyapenda kufanya enzi za uhai wake hasa shughuli zinazowahusu walemavu.
“Mei ni mwezi muhimu kwetu kwa sababu umebeba matukio matatu, kwanza ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu muasisi wetu afariki dunia Mei 2, mwaka 2019 tarehe 18 ndipo taasisi yetu iliposajiliwa rasmi na Mei 29 ni siku ya kuzaliwa kwa dkt. Mengi, hivyo tuna kila sababu ya kuheshimu na kufanya matukio ya kumuenzi” ameeleza Mkurugenzi huyo kupitia taarifa aliyoitoa.
Kwa kushirikiana na Jakaya Kikwete Youth Park na COPE, DRMF wameandaa michezo mbalimbali ya walemavu iliyopewa jina la ” Tembea kwenye viatu vyangu ambapo Makamu wa rais Mama Samia Suluhu atazindua michezo hiyo Mei 1 kwenye viwanda vya Jakaya Kikwete Youth Park.