Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa wahakikishe halmashauri zote nchini zinatumia vizuri mashine na mifumo iliyowekwa katika ukusanyaji wa mapato, huku akisisitiza suala la uadilifu katika ukusanyaji wa mapato
“Lazima suala hili lisimamiwe kwa nguvu zote. Moja ya ajenda kubwa ni mapato, ukusanyaji wa mapato iwe ajenda namba moja katika ratiba zenu za utendaji kazi za kila siku.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo Machi 14, 2022 wakati akizungumza na viongozi hao katika kikao alichokiendesha kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
Majaliwa amesema iwapo hawatasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato bajeti zao hazitoongezeka na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema viongozi hao wanatakiwa wajiridhishe kama watendaji wa halmashauri wanamudu kufikia vyanzo vyote vya mapato, kuviratibu na kutumia mifumo sahihi ya ukusanyaji.
“…Msiwaachie TAMISEMI pekee kusimamia ukusanyaji wa mapato, twende tukasimamie kwenye halmashauri zetu ili kuhakikisha makusanyo hayo yanaongezeka kila siku.”
Sambamba na hayo yote Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Watanzania wajivunie mafanikio yaliyopatika katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani.