Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema sheria za Tanzania zinakataza bayana vitendo vinavyokinzana na tamaduni, mila na desturi na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 Bungeni jijini Dodoma.
Amesema “napenda kuliarifu Bunge lako kuwa sheria zetu hapa nchini, zinakataza bayana vitendo hivyo na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti. Pia, sheria zinakataza kuweka kwenye mitandao maudhui yanayochochea mahusiano ya jinsi hiyo au maonesho ya sanaa yanayochochea vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili yetu.”
Waziri Mkuu amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, ambayo inatamka bayana kuwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja au kinyume na maumbile, iwe kwa faragha au kwa makubaliano ni kosa la jinai.
“Sheria hiyo pia inakataza udhalilishaji wa watoto kwenye matendo yanayofanana na hayo pamoja na kuweka adhabu kwa kosa la kujaribu kufanya vitendo vilivyokatazwa chini ya sheria husika,” amesema.
“Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Tangazo la Serikali Na. 538 la mwaka 2020, zinakataza kuweka mtandaoni maudhui yenye kuonesha mahusiano ya jinsia moja sambamba na adhabu zake na Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 22, inazuia kutangaza au kusababisha machapisho ya ngono au matusi kupitia mfumo wa kompyuta au mfumo mwingine wowote wa kiteknolojia,” ameongeza.
Waziri Mkuu amesema Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018, zinaweka masharti kwamba hakuna kazi ya sanaa itakayopelekwa sokoni kwa walaji kabla ya kupewa kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui yamezingatia maadili. “Baraza katika kuhakiki maadili ya maudhui litajiridhisha kuwa kazi ya sanaa haishawishi wala kuhamasisha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji au matumizi ya dawa za kulevya,” amesisitiza.
Amesema, Serikali imepokea hoja na michango iliyowasilishwa na itaielekeza Tume ya Marekebisho ya Sheria izipitia sheria hizo, kuzifanyia utafiti wa kina na wa kitaalamu ili kubaini mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji na kufanya maboresho.
Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa taasisi zote zilizo na wajibu wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali kama vile Jeshi la Polisi, BASATA na TCRA kutosita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukiuka misingi ya taratibu zetu zilizojiwekwa.