Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid al-Dbeibah ameponea chupu chupu jaribio la kumuua mapema leo wakati watu wasiojulikana walipoishambulia gari yake kwa risasi mjini Tripoli.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al Arabiya, kimeripoti kuwa risasi kadhaa ziliilenga gari ya kiongozi huyo na washambuliaji wakafanikiwa kutoroka eneo la tukio.
Dbeibah alikuwa akirejea nyumbani wakati risasi zilipofyetuliwa kutoka kwenye gari nyingine iliyoondoka kwa kasi ambapo tukio hilo limeripotiwa kwa mwendesha mashitaka mkuu kwa ajili ya uchunguzi.
Iwapo tukio hilo litathibitishwa huenda likachochea mzozo kuhusu udhibiti wa Libya ambako Dbeibah ameshasema atapuuza uchaguzi ulioandaliwa na bunge lenye makao yake mashariki mwa nchi baadaye leo kuchagua waziri mkuu mwingine kuchukua nafasi yake.