Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok, ametangaza kujiuzulu wiki chache baada ya kurejeshwa madarakani katika mkataba wenye utata na majeshi.
Hamdok ametangaza kujiuzulu jana Jumapili ikiwa ni wiki sita tangu aliporejea madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba mwaka jana.
Waziri mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok alipokuwa akitangaza hatua hiyo kupitia televisheni, alisema anaachia wadhifa huo, ili kuruhusu mtu mwingine kusaidia taifa hilo kuvuka katika kipindi cha mpito cha mabadilishano ya kidemokrasia ya madaraka
Aidha, ametoa mwito wa kufanyika kwa majadiliano ili kufikiwa kwa makubaliano mapya kuhusiana na namna serikali hiyo mpya itakavyofikiwa.
Sudan inapita katika kipindi kigumu kinachotishia mustakabali wa taifa hilo, na kulingana na Hamdok juhudi zake za kuliepusha taifa hilo lisitumbukie kwenye janga zaidi hazikufua dafu.
Wanajeshi walichukuwa madaraka Mwezi Oktoba na kumweka Bw.Hamdok chini ya kifungo cha nyumbani, lakini akarejeshwa madarakani baada ya kufikia mkataba wa kugawana na kiongozi wa mapinduzi.
Waandamanaji walipinga makubaliano hayo, wakishinikiza utawala kamili wa kisiasa na kiraia.
Kujiuzulu kwake kunafuatia siku nyingine ya maandamano, ambapo madaktari walisema takribani watu wawili waliuawa.