Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ametangaza kuwa atajiuzulu Juni 7, 2019 kama kiongozi wa Chama Cha Conservative ili kutoa nafasi ya kumchagua Waziri Mkuu mpya.
Kupitia hotuba yake aliyoitoa leo, May amesema kuwa amejaribu kila awezalo kufanikisha kwa usalama matakwa ya wananchi kuhusu taifa hilo kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit) lakini anajuta kwamba hakuweza.
Ameeleza kuwa ataendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo hadi pale kiongozi mpya wa Conservative atakapochaguliwa na hatimaye kumpata Waziri Mkuu mpya.
Chama hicho kimeeleza kuwa kiongozi mpya ataanza kazi kabla ya Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, May atakuwa Waziri Mkuu wakati Rais wa Marekani, Donald Trump atakapoitembelea Uingereza mwanzoni mwa Juni.
Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn amesema kuwa May amefanya jambo jema kujiuzulu na kwamba hivi sasa Conservative inaporomoka.
May anajiuzulu ikiwa ni miaka mitatu tangu apokee kijiti cha aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, David Cameron ambaye pia alijiuzulu.