Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin ametangaza kuwa amepimwa na kukutwa na virusi vipya vya corona (covid-19). Hivyo, amelazimika kuwekwa karantini.
Mishustin amethibitisha taarifa hizo alipokuwa akizungumza kwa njia ya video na Rais Vladimir Putin. Alimpendekeza makamu wake kufanya kazi kama Naibu Waziri Mkuu.
“Imefahamika kuwa vipimo vya virusi vya corona nilivyochukua vimeonesha kuwa nimeathirika, hivyo ninalazimika kujitenga kama sheria inavyoelekeza, na ni lazima nijitenge ili kuwalinda wenzangu,” alisema Mishustin kwenye kipande cha video kilichorushwa pia kupitia ‘Russia 24’.
Rais Putin aliridhia maombi ya Mishustin na kumteua Andrey Belousov kukaimu nafasi hiyo ya Uwaziri Mkuu kama Mishustin alivyopendekeza.
Mishustin amekuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu zaidi nchini humo kutangaza kuwa amepata maambukizi ya virusi vya corona.
Alihudhuria kikao cha baraza la serikali linaloratibu mapambano dhidi ya virusi vya corona uliofanyika juzi, Aprili 29, 2020.
Urusi imefikisha zaidi ya visa 100,000 vya corona hadi kufikia jana, ambapo ilitangaza maambukizi mengi zaidi yaliyopatikana kwa siku moja, yaani visa vipya 7,099. Nchi hiyo imetangaza vifo 1,073 tangu virusi hivyo vilipobainika.