Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar. Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume wamesaini makubaliano ya ushirikiano katika kusimamia na kutekeleza sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuongeza tija.

Uwekaji wa saini za ushirikiano huo umefanyika Jijini Dodoma katika ukumbi wa chuo cha Ufundi Veta, baada ya vikao vya ngazi za wataalam na Makatibu Wakuu wa Wizara husika kuwasilisha taarifa hizo kwa Mawaziri na hatimaye kuridhia tayari kwa ajili ya utekelezaji.

“Hatua hii ni nzuri na muhimu kwetu katika kuhakikisha tunadumisha na kuhifadhi muungano wa kihistoria ambao ulioasisiwa na waasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere na Shehe Amani Abed Karume” amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa katika sekta ya habari ni muhimu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kushirikiana na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ili kuandaa vipindi mbalimbali ikiwemo kipindi cha Utalii Safari chaneli.

Kwa upande wake Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inatangazwa na kuenezwa kuna umuhimu wa kuandaa Kanzi Data itakayojumuisha wataalam wa Kiswahili ambao watakuwa wakifundisha wageni ndani na nje ya nchi.

“Tanzania imechangia sana katika kukuza lugha ya Kiswahili na watu wengi wanapenda kuja kujifunza kwetu ,hivyo naamini kwa kuwa na kanzi data hii itasaidia sana katika kuwapata watalaam wazuri wa kufundisha lugha hii,”amesema Balozi Ally Abeid Karume.

Vilevile Mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha ushirikano katika sekta ya sanaa kwa kuhakikisha kuwa ifikapo Disemba 2019 wanakuwa wamesha andaa kanuni zitakazowawezesha watayarisha wa filamu kutoka nje ya nchi ili kuruhusu utumiaji wa maudhui hayo kwa vyombo vya habari vya serikali.

Pia Mawaziri hao walimalizia kwa kueleza kuwa sekta ya michezo ni sekta muhimu sana katika kutambulisha taifa kupitia michezo mbalimbali na hivyo walikubaliana kuandaa kombe la Muungano, namna bora ya kuibua na kukuza vipaji pamoja na kuteua wajumbe wa bodi ya Baraza laTaifa la Michezo (BMT) na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 3, 2019
Aliyezamia kwenye ndege aripotiwa kufariki Dunia baada ya kudondoka