Ligi ya wanawake inatarajia kuanza kesho Jumapili Novemba 26, 2017 kwenye vituo viwili vya Dar es Salaam na Arusha ambapo kundi A litakuwa Dar es Salaam likitumia Uwanja wa Karume wakati kundi B litakuwa Arusha likitumia Uwanja wa General Tyre.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi  katika mchezo wa uzinduzi wa Ligi Kuu soka ya Wanawake, imefahamika.

Mbali ya Dk. Mwakyembe, wageni wengine wanaotarajiwa kuwa katika uzinduzi huo ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo; Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred pamoja na viongozi wengine wakiwamo Wakuu wa Wilaya mbalimbali za Arusha na mikoa ya jirani.

Kundi A lina timu za Mlandizi Queens ya Pwani, JKT Queens ya Dar es Salaam, Fair Play ya Tanga, Simba Queens ya Dar es Salaam, Ever Green Queens ya Dar es Salaam na Mburahati Queens ya Dar Es Salaam.

Kundi B lenyewe linajumuisha timu za Marsh FC ya Mwanza, Kigoma Sisters ya Kigoma, Panama FC ya Iringa, Baobab Queens ya Dodoma, Alliance Queens ya Mwanza na Majengo Queens ya Singida.

Ufunguzi rasmi wa ligi hiyo utafanyika mkoani Arusha Jumapili Novemba 26, 2017 na mchezo wa ufunguzi utakuwa kati ya Panama FC itakayocheza na Alliance Queens mchezo utakaotanguliwa na hafla ya ufunguzi.

Katika siku hiyo kituo cha Dar Es Salaam kinachotumia Uwanja wa Karume nako kutakuwa na mchezo mmoja utakaowakutanisha Mlandizi Queens dhidi ya JKT Queens.

Maafande wa magereza waikomaliza Young Africans
Video: Majaliwa amlilia Leonidas Gama, ”ametuachia pengo kubwa...”