Waziri wa Nishati Nchini Marekani, Rick Perry, anatarajiwa muda wowote kuanzia hivi sasa kujiengua kutoka katika serikali ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Baadhi vyombo vya habari nchini Marekani vimetangaza kwamba, Waziri huyo amekusudia kujiuzulu nafasi yake hiyo muda wowote kuanzia sasa kutokana na tuhuma za kuhusishwa kutoa vibali sita vya siri kwa mashirika ya Kimarekani kwa ajili ya kuiuzia Saudi Arabia teknolojia ya nyuklia.
Taarifa za siri kutoka ikulu ya Marekani White House pia zinasema kwamba,Perry amekuwa akifuatilia taratibu za kujiuzulu kwake kwa muda wa wiki sasa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hadi sasa White House haijatoa taarifa yoyote kuhusiana na habari hiyo.
Inaelezwa kwamba awali Trump alikuwa amemtaka Rick Perry kushika hatamu za Wizara ya Usalama wa Ndani nchini Marekani, lakini kiongozi huyo alitupilia mbali ombi hilo.
Mwezi Machi mwaka huu kuliripotiwa kwamba Waziri huyo wa Nishati alihusika kutoa vibali sita vya siri kwa mashirika ya Kimarekani kwa ajili ya kuiuzia Saudi Arabia teknolojia ya nyuklia na kuisaidia nchi hiyo katika masuala hayo.
Perry alitoa vibali hivyo katika hali ambayo Saudi Arabia inakosolewa kote duniani kutokana na ukiukaji wake wa wazi wa haki za binaadamu na mauaji yake nchini Yemen, mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa serikali ya Saudia, aliyeuawa tarehe 02 Oktoba mwaka jana ndani ya ubalozi mdogo mjini Istanbul, Uturuki.