Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ametoa maelekezo manne kwa wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa lengo la kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Waziri Ndaki amewaeleza wataalam hao kuwa viongozi wataendelea kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha lengo linafikiwa, hivyo amewataka wataalam hao kuwa waaminifu, waadilifu na kufanya kazi kwa kujitolea.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda amewataka wataalam hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu lakini pia watalazimika kuwajibika kutokana na matendo yao kwenye suala la ukusanyaji wa mapato. Vilevile amewataka kuhakikisha wanakusanya mapato katika maeneo yao na kucha tabia ya udanganyifu kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao. Adiha, amewataka wataalam hao kuwasilisha taarifa za makusanyo kila mwezi.
Kaimu Mkuu wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo – Iringa, Bw. Rajon Deule amesema kuwa sababu ya kituo chao kufanya vizuri ni kwamba Kanda yao wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara ambavyo huwa wanajadili changamoto wanazokutana nazo na kujiwekea mikakati ya namna ya kukabiliana nazo. Kwa kutumia njia hiyo imewasaidia kuweza kukusanya maduhuli ya serikali vizuri.