Eva Godwin – Dodoma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amewasimamisha kazi watumishi 11 waliokuwa wakifanya kazi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mwanza, kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Silaa amechukua maamuzi hayo hii leo Jijini Dodoma Oktoba 23, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza hatua inalenga kuboresha sekta ya ardhi nchini huku akiielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kufanya uchunguzi dhidi ya watumishi hao na kuchukua hatua.

Amesema, “Oktoba 3, mwaka huu, Serikali ilitoa maelekezo yaliyolenga kuboresha sekta ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mwanza ambapo wizara imeanza kuchukua hatua, tumewasimamisha kazi watumishi wawili waliokuwa wakifanya kazi Mwanza na watumishi tisa wa Jiji la Dodoma kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.”

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.

Silaa ameongezea kuwa Wizara inaendelea na uboreshaji wa Mifumo ya Kielekroniki wa Kutunza Taarifa za Ardhi (ILMIS) ili kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa hati milki na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao.

“Maboresho ya mfumo huo yanatarajiwa kukamilika mwaka huu mwishoni na kusambazwa nchi nzima, na hii itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutunza taarifa za ardhi na pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na ofisi ya ardhi waliendesha kliniki maalumu na jumla ya wananchi 3,056 walihudumiwa. Hati milki 1,474 zilitolewa papo hapo na utaratibu huu umekuwa ukitekelezwa nchi nzima,” amesema Silaa.

Chemba kufuatilia, kuimarisha vyanzo vya mapato
Maadhimisho miaka 78 ya UN Oktoba 24