Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali za rufaa za mikoa nchini kuboresha huduma za afya pamoja na kuwa na mawazo mapana katika kuboreshaji miundombinu ya hospitali hizo ili kuweza kuisaidia na kuipunguzia mzigo hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
Hayo yamesemwa leo na Waziri Ummy wakati akiongea na wafanyakazi wa idara ya tiba ikiwa ni mwendelezo wa kukutana na kufanya mapitio ya idara mbalimbali zilizopo kwenye wizara hiyo
Waziri Ummy amesema ili kuonesha kweli idara ya tiba ndio inayobeba wizara hiyo hamna budi kuboresha huduma hizo ili zilingane na mahitaji ya wananchi kwani wananchi wanaziamini hospitali za umma.
“Tunatakiwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya ni mzuri, hivyo ni wakati wa kuangalia changamoto na kuziboresha ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wanafika kwenye vituo vyetu kupata huduma“ Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri huyo ameitaka idara hiyo kufanya upya mapitio ya miongozo ya utoaji huduma ili kufanya huduma zinazotolewa kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa zinakuwa bora na zenye manufaa kwa wananchi vilevile miongozo hiyo iweze kuunganisha vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hata hivyo Waziri Ummy amewataka watumishi wa idara hiyo kufanya kazi kama timu na endapo kuna changamoto ni vyema zikajadiliwa kwa pamoja ili kwenda kwa pamoja katika kuboresha huduma za afya nchini.