Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewasimamisha kazi wiki mbili watumishi Wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupisha uchunguzi tuhuma za ubadhirifu ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa.

Ameyasema hayo leo Mei 28, alipofanya ziara kwenye ujenzi wa mradi wa machinjio hayo ya mifugo ya kisasa, mara baada ya kupewa taarifa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi na kuonekana kuna ubadhirifu wa fedha.

“Kuna watumishi wengine najua wameshahamishwa hapa Shinyanga, hivyo naagiza waletwe hapa ili kujibu tuhuma za ubadhirifu wa ujenzi wa machinjio hii ya mifugo ya kisasa, pamoja na Wakandarasi wachukuliwe hatua,” amesema Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa gharama za ujenzi wa machinjio hiyo anazifahamu ni Shillingi bilioni 5.7 na zimeshatumika bilioni 5.1 na kuhoji juu ya Shillingi milioni 600 mahali zilipo, huku mradi huo ukiwa bado haujakamilika na kutakiwa tena kuongezwa Shillingi Milioni 172 kutoka kwenye mapato ya ndani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemoni Sengati, amesema suala la watumishi hao atalifanyia kazi na watatoa taarifa ndani ya wiki mbili ambazo zimetolewa.

Albam ya DMX yakamilika siku 48 baada ya kifo chake
Watuhumiwa 12 mbaroni kwa wizi, ushirikina