Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ataweka usawa kwa Madaktari juu ya fedha wanayolipwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya – NHIF, kwamba Daktari anayelipwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na mfuko huo, anatakuwa akilipwa sawa na wa Wilayani.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa uhitimishaji wa ziara yake ya siku tatu ya kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza, Halmashauri, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati Kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto pamoja na upatikanaji wa Dawa na Vifaa tiba.
“Daktari anayelipwa Muhimbili na NHIF ndio tunataka alipwe sawa na Daktari aliyopo Wilayani sababu wote wanasifa sawa ili wanaokaa Wilayani nao waone raha ya kusoma kwa shida, kupambana hadi kuwa Daktari,” alisema Waziri Ummy
Katika ziara hiyo, Waziri Ummy amesisitiza juu ya utolewaji wa huduma bora kwa kuzingatia Weledi, Maadili ya Taaluma ya Udaktari kwa kufuata miongozo ya utoaji wa huduma pamoja na upatikanaji wa dawa katika na kuongeza kuwa Serikali inawapambania kupata haki zao na wao wapambane kutoa huduma bora.