Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameitaka jamii kuwajibika kuwawezesha wazazi, hususa wanawake kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Duniani, yaliyofanyika Wilayani Muheza Mkoani Tanga.
Amesema watoto wanapotimiza miezi sita waanzishiwe vyakula vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili.
Waziri Ummy ameeleza kuwa idadi ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza kwa wakati katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 87 na idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6-23 wanaolishwa chakula vigezo vya ubora kilishe ni asilimia 35.
”Vigezo hivyo ni idadi sahihi ya milo anayopewa mtoto kwa siku kulingana na umri wake na mlo uwe na mchanganyiko wa vyakula kutoka kwenye makundi yasiyopungua manne ya vyakula” Amesema Waziri Ummy
Kauli mbiu ya Wiki ya Maadhimisho ya Unyoynyeshaji duniani mwaka 2020 ni ‘Tuwawezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa Mazingira’.