Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotatua kero za wananchi.

Ameyasema hayo Leo Agosti 10, 2021 katika ziara ya kikazi aliyoianza mkoani Njombe, ambapo pamoja na mambo mengine atakagua miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya ngazi ya msingi, sekta ya elimu na ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Waziri Ummy, amesema Sekretarieti za Mikoa zina wajibu wa kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatimiza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa wananchi wanahitaji kupatiwa maendeleo na maendeleo yanapatikana kwa Halmashauri imara.

Katika ziara hiyo, Waziri Ummy amesisitiza umuhimu wa viongozi wa sekretarieti za Mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia kwa weledi ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani mwaka wa fedha 2021 / 2022 kwa kuwa ndio wasimamizi wakuu katika ngazi ya Halmashauri.

Hata hivyo amesema kuwa Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa wana wajibu wa kuhakikisha wanachambua bajeti za halmashauri na kuangalia vipaumbele ambavyo vinasaidia katika kutatua kero za wananchi zikiwemo ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na ujenzi wa miundombinu ya Barabara.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 11, 2021
RITA imesajili watoto chini ya miaka 5 kwa asilimia 55