Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameagiza waganga wakuu wa Mikoa, wa Wilaya na Waganga wafawidhi kuweka matangazo katika vituo vya afya, Zahanati na Hospitali kwamba huduma za upimaji na matibu ya Malaria ni bure na wananchi hawatakiwi kulipia kwakuwa kuna wafadhili wanao gharamia gharama hizo.
Waziri Ummy ametoa maagizo hayo Mkoani Kigoma katika Zahanati ya Mwandiga wakati akizindua ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu kwa wakina mama wajawazito na watoto wenye umri wa mwaka moja kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya kitengo cha kudhiti malaria na Shirika la misaada la marekani (USAID).
Waziri Ummy ameeleza kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kutozwa fedha kwa ajili ya matibabu huku Serikali imeagiza kuwa zoezi hilo ni bure.
Amesema ugawaji endelevu wa vyandarua ni mradi unaoendeshwa kwa pamoja na shirika la ‘JohnsHopkins Center for Communication’ na ‘Vectorworks’ kwa ufadhili wa shirika la misaada la Marekani (USAID) kupitia mfuko wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti Malaria na kuratibiwa na Serikali kupitia Mradi wa Kupambana na Malaria (NMCP) kwa hiyo vyandarua hivyo ni bure na Wananchi wanatakaiwa wasilipie.
Aidha, Waziri Ummy amesema ofisi ya takwimu (NBS) katika Kaya mwaka 2017 zilionyesha kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya Malaria hadi chini ya asilimia 10% kutokana na mikakati iliyowekwa na Wizara kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa Malaria.
Amesema mikakati ya Serikali ni kuongeza kasi ya upimaji wa Malaria kwa kutumia kipimo cha (mRDT) Hadubini na kutumia dawa za mseto pindi wanapothibitika kuwa na vimelea vya malaria, kuwapatia wajawazito vyandarua vyenye viuatilifu ili kujikinga kuumwa na mbu pia kuwapatia dawa za ‘Sp’ kwa kipindi maalumu wakati wa ujauzito ilikuwakinga na madhara yatokanayo na Malaria.
“Niendelee kusisitiza dawa za malaria na matibabu ni bure wananchi hawatakii kulipia, wafadhiri wetu wanajitoa sana kuhakikisha suala la Malaria liishe, waganga wafawidhi wanatuangusha sana niombe muweke matangazo na namba za simu kwenye vituo vya afya iliwananchi watakao lipishwa watoe malalamiko yao ilikuweza kuondokana na changamoto ya ugonjwa wa Malaria”, amesema Waziri Ummy.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Wilaya ya Kigoma Vijijini, Elisha Robarti amesema zahanati hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi kwani wanahitaji ni watumishi 15 na waliopo ni watumishi 7 hali inayopelekea watumishi kulemewa.
Pia, wananchi waliofika kupata huduma katika zahanati hiyo mbele ya Waziri Ummy, Lydia Leonard amesema wamekuwa wakitozwa shilingi 2500/= kwa ajili ya Kipimo cha Malaria na kulipa dawa wanapofika kwa ajili ya matibabu .
Amesema pamoja na kuwa na Kadi ya bima ya Afya lakini bado wanaendelea kutozwa fedha na kumuomba Waziri kusimamia suala hilo iliwaweze kupata Matibabu bure kama serikali inavyo elekeza.
Hata hivyo, wananchi hao wameiomba Serikali kuwajengea kituo cha afya, Kata ya Mwandiga pamoja na kuboreshewa huduma za maji kwani maji wanayo yatumia sio salama na wanalazimika kutumia Kilomita 13 kufuata huduma.
Kufuatia hayo, Waziri ametoa maelekezo kwa halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Vijijini kuanza ujenzi wa kituo hicho kwa kuwa Kata hiyo inawatu wengi na inahitajika kupata kituo cha Afya.