Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel nchini Tanzania Mhe. Yahel Vilan ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamekubaliana kuanzisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ambayo yatazinufaisha Tanzania na Israel katika sekta ya Afya.

Balozi huyo anayezihudumia nchi za Afrika mashariki zikiwemo Kenya na Uganda katika mazungumzo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameyataja  baadhi ya mambo ambayo Israel imekuawa ikishirikiana na Tanzania kuwa ni pamoja na utaratibu wa kuleta madaktari  wa kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na ujuzi kwa wataalaam.

Balozi Yahel amesema Israel imekua ikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam hususani madaktari na Wauguzi kutoka Tanzania na kuongeza kuwa wanao mpango wa kusaidia uanzishwaji wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika eneo ambalo serikali ya Tanzania itapenda kuboresha huduma hiyo.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Serikali kwa misaada hiyo na mashirikiano mapya yatakayoanza kati ya Israel na Tanzania kwenye sekta ya Afya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema anaishukuru Serikali ya Israel kwa misaada mikubwa inayotoa katika eneo la tiba hasa matibabu ya wagonjwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete.

Amesema madaktari bingwa wanaotoka katika nchi mbali mbali ikiwemo Israel wamekuwa wakitoa huma ya upasuaji katika taasisi hiyo na kuisaidia Serikali kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

“Hadi sasa kati ya wagonjwa 400 waliokuwa wanasubiri kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu nusu yao wamepatiwa matibabu kupitia mashirikiano haya” Amesema Mhe. Ummy.
Kwa upande wa mafunzo Mhe. Ummy Mwalimu ameshauri yatolewe kwa kada nyingi zaidi ikiwemo wataalam wa maabara,wauguzi, madaktari na kadhalika ili kuhakikisha lengo la serikali la kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi linafanikiwa.
Akizungumzia ombi la balozi huyo la Israel kutaka kusaidia ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahututi, hapa nchini Mhe.Ummy amependekeza chumba hicho kijengwe Dodoma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Amesema sababu za mapendekezo hayo zimetokana na uamuzi wa serikali wa kuhamia Dodoma ambao unakwenda sambamba na maboresho makubwa ya utoaji wa huduma za afya kwa watu watakaohamia Dodoma.

Aidha, amefafanua kuwa wataalam kwa ajili ujenźi wa chumba hicho wanatarajia kufika nchini mwezi septemba kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa ahadi ya balozi huyo

Tume Ya Mipango Yaendesha Mafunzo Ya Uwekezaji Wa Umma
Kumuangalia mwanamke zaidi ya sekunde 14 ni kosa India, wanawake watakiwa kujifuza karate